01 February 2013

Pinda ataka amani itawale Mtwara



Goodluck Hongo na Rose Itono

WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, amesema Serikali haitawachukulia hatua viongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi
wanaotuhumiwa kusababisha vurugu zilizotokea mkoani Mtwara, kusababisha vifo na uhalibifu mkubwa wa mali bali jambo la msingi
ni kuhakikisha amani inatawala mkoani humo.


Vurugu hizo zilichangiwa na maandamano ya wananchi waliokuwa wakipinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

Bw. Pinda aliyasema hayo katika kipindi cha maswali na majibu bungeni mjini Dodoma jana baada ya kuulizwa swali na Kiongozi
wa Kambi ya Upinzani bungeni, Bw. Freeman Mbowe ambaye pia
ni Mbunge wa Jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro.

Katika swali lake, Bw. Mbowe alitaka kujua hatua ambazo Serikali itazichukua kwa viongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi ambao kauli zao zimechangia vurugu hizo kwa namna moja au nyingine.

Alisema kilichotokea mkoani humo ni matokeo ya mahusiano hafifu kati ya wananchi na Serikali ambapo hata kauli za viongozi wa CCM nazo zilichangia vurugu hizo je, kwanini wasichukuliwe hatua.

Msingi wa swali hilo ulitokana na malalamiko ya wananchi ambao waliitaka Serikali iwaondoe baadhi ya viongozi mkoani humo kwa kupingana na madai yao ya kutokana gesi hiyo isisafirishwe.

Akijibu swali hilo, Bw. Pinda alisema Serikali haiwezi kuwachukulia hatua ili kuepusha lawama hasa ukizingatia
kuwa, tayari kilio cha wananchi kimesikilizwa.

“Nilikwenda Mtwara nikakutana na viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini, Serikali na wananchi ambapo walitoa maoni yao bila kificho na kuitak Serikali iwaondoe baadhi ya viongozi ambao walikuwa kikwazo kutokana na kauli zao,” alisema Bw. Pinda
ambaye majibu yake yalionekana 'kuwakuna' wabunge wa CCM.

“Niwaombe Watanzania wenzangu, viongozi na wanasiasa, jambo hili limekwisha hivi sasa tuongee lugha moja ya amani...kwani Tanzania ni moja,” alisema Bw. Pinda.

Alisema kutokana na vurugu hizo, baadhi ya kampuni ambazo zimewekeza mkoani humo zimeingiwa na hofu na nyingine
kuomba kukaa miezi mitatu bila kufanya shughuli zao hadi watakaporidhika na hali ya utulivu.

Bw. Pinda alitomia fursa hiyo kutoa pole kwa watu waliofikwa na matatizo ambapo Serikali itaangalia uwezekano wa kuwasaidia.

1 comment:

  1. WAZIRI MKUU ULIAHASHIDI WALIOCHOCHEA MACHAFUKO UTAWASHITAKI KWENYE CHAMA USIISHIE KUTOA KAULI TU

    ReplyDelete