01 February 2013

Mvua yaua mwanafunzi, yajeruhi


Na Yusuph Mussa, Korogwe

MVUA kubwa iliyoambatana na upepo mkali imeleta maafa katika Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, baada ya kuua mwanafunzi mmoja wa sekondari, kujeruhi, kuezua paa za nyumba, mabweni
na madarasa ya Shule ya Sekondari Mkalamo iliyopo Kata ya Magamba-Kwalukonge, Tarafa ya Mombo.


Akizungumza na Majira kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Constantine Masawe, alisema tukio hilo limetokea juzi saa 11.45 jioni ambapo wanafunzi waliojeruhiwa wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya, Magunga.

Majeruhi hao ni Salma Bakari (15), ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Mkalamo aliyevunjika mguu
wa kulia, Omar Haji (13) na Catherine Albert wa Shule ya Msingi Magamba- Kwalukonge na Asha Bakari wa Sekondari ya Mkalamo.

Albert aliumia kichwani, Haji (mgongo na mbavu) wakati Bakari  aliumia mguu wa kushoto baada ya kukimbilia katika nyumba ya Bw. Mustapha Abdallah ndipo walipopigwa na miti, mabati, kuangukiwa na ukuta.

Alisema bweni moja la wasichana katika Shule ya Msingi Magamba- Kwalukonge, limeanguka kabisa na jingine likitoa
nyufa ambapo madarasa mawili ya Sekondari ya Mkalamo
yameezuliwa paa zake.

“Inaaminika bado kuna nyumba nyingine zimeanguka au kuezuliwa paa zake na upepo lakini tutatoa taarifa kadiri muda unavyokwenda,” alisema Kamanda Masawe na kuongeza kuwa,
inaaminika nyumba nyingine za wenyeji zimekwenda na upepo
kwenye Kijiji cha Magamba Kwalukonge.

Wakati huo huo, mvua hiyo imesababisha kifo cha mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Semkiwa, iliyopo Mtaa
wa Mtonga, mjini Korogwe, mkoani Tanga, Patrick Paul (14).

Mwanafunzi huyo amefariki dunia jana katika Hospitali
ya Wilaya, Magunga wakati akiendelea kupatiwa matibabu
baada ya upepo mkali ulioambana na mvua kumuangusha
akiwa juu ya mti.

Mvua hiyo pia imeezua paa katika nyumba tisa zilizopo mitaa
ya Mtonga na Kwamkole. Taarifa iliyotolewa na Ofisa Mtendaji Kata ya Mtonga ambayo Majira inayo nakala yake, Bw. Maurice Kinyashi, ilisema tukio hilo limetokea juzi saa 12 jioni.

Alisema pamoja na mvua hiyo kusababisha kifo cha mtu mmoja,
mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Semkiwa, Rahim Ramadhani amejeruhiwa baada ya kuangukiwa na paa wakati mtoto wa miaka mitatu, Halifa Shabaan, alifunikwa na paa lakini hakuumia.

“Ukuta wa Kanisa la TAG nao ulianguka, hivi sasa waathirika wote wapo katika wakati mgumu wakiishi katika nyumba ambazo hazina paa,” alisema Bw. Kinyashi.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment