01 February 2013

Mkakati wa kumtoa Ponda waandaliwaNa Rehema Mohamed

WAKATI Katibu wa Taasisi za Jumuiya za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda na Shekhe Swaleh Mkadam, wakiendelea kusota rumande baada ya kunyimwa dhamana na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), wafuasi wao wamepanga kufanya kongamano maalumu la kujadili namna ya kuwatoa washtakiwa hao.

Shekhe Ponda na wenzake wanakabiliwa na kesi ya uchochezi pamoja na wizi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambapo dhamana zao zimefungwa kwa sababu za kiusalama.

Jana kesi hiyo ililetwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusikilizwa
na baada ya kuahirishwa, wafuasi hao walionekana wakigawana vikatarasi vilivyokuwa na ujumbe wa kufanya kongamano hilo.

Vikaratasi hivyo vilikuwa na ujumbe uliowataka Waislamu wote nchini kukutana Februari 3 mwaka huu, saa 8 mchana eneo la Temeke kwenye kiwanja cha Nurul Yaqiin (Uwanja wa Pumba) karibu na Uwanja wa Mwembeyanga.

Ujumbe huo uliongeza kuwa, kitendo cha washtakiwa hao kuendelea kunyimea dhamana ambayo ni haki yao, kinawafanya waendelee kuteseka kwa sababu ya kutetea mali za Waislamu ambazo
zinaendelea kuuzwa na kupolwa.

Pia ujumbe huo uliwataka Waislam wajumuike pamoja, kuonesha mshikamano wao na kutoa maamuzi ya pamoja juu ya nini cha kufanya ili haki itendeke kwani Muislamu wa kweli hawezi
kukubali dhuruma yoyote dhidi yake.

Wakati huo huo, akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo, shahidi wa sita Bw. Hamis Mkangama (30), aliieleza mahakama hiyo kuwa Shekhe Ponda aliwakataza wasiendelee na ujenzi wa uzio katika
kiwanja kinachodaiwa kuvamiwa.

Bw. Mkangama ambaye ni fundi mwashi, alisema yeye na wenzie 20 walikuwa wakichimba msingi wa uzio kwenye kiwanja cha
Markaz ambapo Shekhe Ponda na wenzake, walikwenda eneo
hilo na kuwahoji aliyewapa idhini ya kujenga eneo hilo.

“Tulimjibu kuwa bosi wetu Selemani ndiye aliyeturuhusu kujenga
na kututaka tusitishe ujenzi akidai kiwanja husika kina mgogoro,” alidai shahidi huyo.

Aliongeza kuwa, pamoja na kuambiwa wasimamishe ujenzi wao waliendelea ndipo Shekhe Ponda, aliamua kupiga picha eneo hilo.

Alidai kuwa, walimweleza bosi wao juu ya suala la Shekhe Ponda ambaye aliwataka wasitishe ujenzi huo na kudai kuna matatizo yameanza kujitokeza.

Wakati Shekhe Ponda akiondoka katika viwanja vya mahakama hiyo akiwa ndani ya gari la Magereza, wafuasi wake walimuaga kwa kunyoosha mikono wakisema 'Takbirr -alahu akbar', wengine
wakilikimbiza gari hilo hadi barabarani.


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 14 mwaka huu kwa
ajili ya kutajwa na Februari 18 kwa ajili ya kusikilizwa.

1 comment:

  1. MAHAKAMA IWE NA UANGALIFU ISIWAHAMASISHE WATANZANIA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI WASLAMU WASIFIKIRI WAKRISTO NI MBUMBUMBU IWAPO WALIWAACHIA WAKACHINJA NG'OMBE NA VITOWEO VINGINE SI KWAMBA WAKRISTO HAWAWEZI KUCHINJA KITOWEO

    ReplyDelete