18 February 2013

Mganga akutwa na mkono wa albino *Utapelekwa mahakamani kama ushahidi



Na Prosper Mgimwa, Sumbawanga

JESHI la Polisi mkoani Rukwa, linamshikilia mganga wa kienyeji aliyefahamika kwa jina moja la Kaponda kwa tuhuma ya kukutwa
na mkono wa mlemavu wa ngozi 'albino', katika Kijiji cha Miangalua, wilayani Sumbawanga.


Mganga huyo alikamatwa jana kijijini hapo baada ya Jeshi la Polisi kupewa taarifa na wasamalia, kwenda eneo la tukio (nyumbani kwake) na kufanikiwa kuukuta mkono huo ambao aliuficha.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Jacob Mwarwanda, alisema
mkono huo umehifadhiwa katika chumba cha maiti kwenye
Hospitali ya Mkoa kwa ajili ya ushahidi mahakamani.

“Mlemavu wa ngozi aliyekatwa mkono huu anaitwa Mary Chambanenje ambaye amelazwa katika hospitali hii ya Mkoa
akiendelea kupatiwa matibabu na madaktari,” alisema.

Aliongeza kuwa, mganga huyo atafikishwa mahakamani muda
wowote baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika ili sheria
iweze kuchukua mkondo wake.

Hata hivyo, Kamanda Mwarwanda alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na jeshi hilo ili kufichua vitendo vya uhalifu na
ukatili vinavyofanywa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.

No comments:

Post a Comment