01 February 2013

Madiwani Kigamboni waponzwa na mwaliko wa TibaijukaNa Andrew Ignas

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Temeke, limemtaka Meya wa halmashuri hiyo, Bw. Maabadi Hoja, awachukulie hatua za kinidhamu madiwani wa Kigamboni waliokubali mwaliko wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Hali hiyo inatokana na madiwani hao kuridhia kuundwa kwa Kamati Maalumu ya kusimamia mradi wa Mji Mpya wa Kigamboni bila kumshikilisha Mwenyekiti wa halmashauri hiyo na madiwani wa Temeke ili kutetea haki na masilahi ya wananchi.

Wakizungumza katika kikao cha baraza hilo kilichokuwa kikijadili ajenda mbalimbali za halmashauri, madiwani hao akiwemo Bw. Wilfred Kimati (Kata ya Kurasini) na Naibu Meya Bw. Noel Kipangule (Kata ya Chang'ombe), walisema umefika wakati
wa Bw. Hoja kuonesha makucha yake kwa madiwani hao.

Walisema madiwani hao wameonesha usaliti mkubwa kwa
kukubali mwaliko huo na kuridhia uundwaji wa kamati hiyo.

“Suala hili kama tutalifumbia macho, litaleta vita kwa sababu kama madiwani wa Temeke tumetelekezwa, itakuwa vigumu wananchi kupata taarifa za jambo hili ndio maana tunamuomba Meya
atoe adhabu kwa madiwani hawa,” walisema.

Waliongeza kuwa, licha ya kuundwa kamati hiyo bado Serikali ilitakiwa kuwashirikisha madiwani wa Temeke ili waweze kuzungumza na wananchi wao.

Diwani wa Kata ya Makangalawe, Bw. Victor Mwakasindile, Prof. Tibaijuka anapaswa kuandaa semina maalumu itakayoshirikisha madiwani ili waweze kutoa elimu kwa umma juu ya mradi huo
ili kuepukana vurugu kama zilizotokea mkoani Mtwara.

“Kama mradi utahusisha maeneo ambayo wananchi wanyamiliki kihalali, madiwani wanapoulizwa watashindwa kutoa majibu hivyo ipo hatari ya kutokea vurugu,” alisema Bw. Mwakasindile.

No comments:

Post a Comment