01 February 2013

Ligi Kuu ya Grand Malt kuanza leoNa Mwandishi Wetu, Zanzibar

MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu ya Zanzibar maarufu zaidi kwa jina la Grand Malt Premier League, unatarajiwa kuanza leo kwa michezo miwili kati ya Mafunzo na KMKM zitakazokwaana Uwanja wa Amaan, huku Chipukizi na Falcon wakioneshana kazi Uwanja wa Gombani, Pemba


KMKM wanaingia uwanjani wakitaka kuendeleza ubabe wao, kwani mpaka sasa ndiyo wanaoongoza ligi hiyo wakiwa wamejikusanyia pointi 23, wakati Mafunzo ikiwa nafasi ya pili ikiwa na pointi 22.

Ugumu wa mchezo huo ni kuwa kila timu itataka kujiimarisha zaidi kwani kuteleza ni kujiweka katika mazingira magumu ya kutwaa taji na iwapo KMKM, itakubali kichapo, itaichia Mafunzo kushika usukani wa ligi hiyo yenye timu 12.

Chipukizi wao watataka kuutumia vyema uwanja wa nyumbani, kwani ikiwa nafasi ya tano kwa pointi 17 ilizonazo itataka kuhakikisha inashinda, ili kuzidi kupaa katika msimamo wa ligi hiyo ambayo kwa sasa imeongezeka mvuto kutokana na udhamini wa Grand Malt.

Hata hivyo wasitegemee mteremko kutokana na Falcon, nayo kutaka kujinasua kutoka nafasi za chini. Kwa sasa timu hiyo inashikilia nafasi ya tisa ikiwa na pointi 13.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena kesho, kwa michezo miwili wakati Bandari na Malindi zitakapokwaana Uwanja wa Mao, huku Jamhuri na Duma zikioneshana ubabe Uwanja wa Gombani, Pemba na Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja kati ya Zimamoto na Mtende zitakazocheza Uwanja wa Mao.

Timu inayoshika mkia mpaka sasa ni Mundu ikifuatiwa na Malindi. Timu zote hizi zina pointi saba kila moja.

No comments:

Post a Comment