05 February 2013

Kikwete: Serikali itafanyiakazi mapendekezo ya APRM


Na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa Serikali yake itafanyiakazi mapendekezo juu ya namna ya kuboresha baadhi ya maeneo ya utawala bora kama
ilivyoainishwa na Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).

Wiki iliyopita, Marais Kikwete na Michael Sata wa Zambia waliwasilisha na kujadiliwa ripoti za nchi zao chini ya utaratibu wa APRM kwenye kikao cha
Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika Wanaoshiriki Mchakato wa APRM.

Akizungumza katika hotuba yake kwa wananchi chini ya utaratibu aliojiwekea ya mwisho wa mwezi Januari iliyosomwa Ijumaa jioni, Rais alieleza safari
yake ya nchini mbalimbali na kugusuia juu ya Tanzania kuwasilisha ripoti ya APRM.

“ Nchini Ethiopia tulishiriki katika mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika na katika kikao cha African Peer Review Mechanism (APRM) ambapo taarifa ya tathmini ya utawala bora ya Tanzania na Zambia iliyofanywa na APRM ilijadiliwa,” alisema.

Rais aliongeza kuwa katika kikao hicho Tanzania ilifanya vyema ambapo viongozi wa nchi nyingi za Afrika waliridhishwa na hali ya utawala bora
Tanzania na kuitaja kuwa nchi ya mfano katika masuala mengi.

Rais alisema kuwa sasa Serikali yake itakaa kuyachambua mapendekezo yaliyotolewa kwa lengo la kuhakikisha kuwa maeneo yenye changamoto
yafanyiwakazi katika Mpangokazi ulioandaliwa.

“Kwa jumla hatuna mahali tuliponyooshewa kidole kuwa tunafanya vibaya.Tumepongezwa katika mambo mengi na tumepewa ushauri kwa baadhi ya maeneo
waliyoona hatuna budi kuyaboresha. Nilipata nafasi ya kusema ambayo niliitumia kufafanua baadhi ya mambo yaliyokuwamo kwenye taarifa.

Niliwashukuru na kuahidi kuufanyia kazi ushauri uliotolewa. Tathmini ya nchi yetu ilipitishwa kwa kauli moja," alisema Rais.

APRM iliasisiwa mwaka 2003 ambapo hadi sasa zimefikia nchi 33 kati ya 54 za Afrika zimeridhia kuwa na chombo hicho cha kutathimini utawala.

Nchi kama Kenya, Uganda, Rwanda, Msumbiji, Afrika Kusini, Liberia, Gahana na nyinginezo ni baadhi ya zilizoona umuhimu wa kujiunga na taasisi hii.

APRM Tanzania ilianza kufanyakazi mwaka 2007 baada ya kuwa nchi ilisaini mkataba mwaka 2004 na kukubali kuanzisha chombo hicho hapa nchini kwa ajili ya kufanya utafiti juu ya utawala bora kwa wananchi.

Mpango wa Bara la Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) japo ndio uko katika siku za kwanza za utekelezaji lakini umeweza kufanya kazi nzuri
sehemu mbalimbali Afrika ambapo hapa nchini Serikali imekuwa ikiufadhili kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.


No comments:

Post a Comment