05 February 2013

Kandoro akerwa na watendaji


Na Charles Mwakipesile, Mbeya

MKUU wa Mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro, amewashukia watendaji wa Serikali wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao
na kuwafanya wananchi wapeleke kezo zao ofisini kwake.


Bw. Kandoro aliyasema hayo juzi usiku katika hafla ya kuukaribisha mwaka 2013 ambapo hafla hiyo ilihudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Maofisa wa ngazi mbalimbali, watumishi serikalini
na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara.

Alisema ni hatari kubwa kuona viongozi wa Serikali wanakosa majibu ya kuwapa wananchi wanaowafuata katika ofisi zao hivyo kuamsha hasira na vurugu zisizo za lazima.

“Mwaka huu wa 2013, nataka tuache tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na kuzizoea ofisi zetu, tuwe na majibu ya uhakika kwa wananchi ili kutatua kero zao...wao ndio waaajiri wetu na sisi
ni watumishi wao,” alisema Bw. Kandoro.

Alionesha kukerwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri, kushindwa kutatua matatizo ya wananchi.


Alishangazwa na baadhi ya watu kutaka kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini bila sababu za msingi kwa kuanzisha vurugu za kidini na kusisitiza kuwa, hatawavumilia watu ambao watataka kuvuruga amani mkoani humo bali atawafikisha katika vyombo vya sheria.

“Kila mwana Mbeya aone fahari ya Mkoa huu kutunza amani hivyo fanyeni kazi kwa bidii na kuheshimiana ili kustawisha uchumi wetu ambao unakua siku hadi siku,” alisema.

Mwenyekiti wa Wazee mkoani humo, Mzee Isakwisa Mwambulukutu, alimpongeza Bw. Kandoro kwa kuufanya
Mkoa huo upate maendeleo yanayokua siku hadi siku.

“Jambo la msingi kila kiongozi aliyepo mahali hapa, awajibike kufanya kazi zake kwa bidii na uadilifu mkubwa ili kuufanya
Mkoa wetu usonge mbele kimaendeleo,” alisema.

No comments:

Post a Comment