05 February 2013

Kagesheki ahimiza utunzaji wa vyanzo vya maji


Na Stella Aron

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Khamis Kagasheki
amewahimiza wananchi kutunza vyanzo vya maji na kuacha kufanya shughuli zozote katika sehemu hizo ili kuepuka uharibifu.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa wizara hiyo George Matiku, alisema kauli hiyo aliitoa jana katika maadhimisho ya siku ya Ardhioevu Duniani ambayo hufanyika kika ifikapo Februari 2, kila mwaka.

"Katika siku hii watu duniani kote wanatafakari na kukumbushana umuhimu wa Ardhioevu katika maisha yao ya kila siku na kauli mbiu ya siku ya Ardhioevu ‘Ardhioevu hutunza maji’. Hii ni kutumbukusha nafasi ya ardhioevu katika kuhakikisha kuwa maji yanakuwepo siku zote na kwa vizazi vyote, " alisema.

Matiku alisema kuwa siku ya ardhioevu Duniani inaadhimishwa Kitaifa mjini Babati Mkoani Manyara ambako Mkuu wa Mkoa alikuwa mgeni rasmi ambapo maandalizi hayo yameandaliwa na klabu za Malihai kutoka shule za Msingi, Sekondari na vyuo mbalimbali.

Alisema kuwa katika siku hiyo kutakuwa na shughuli mbalimbali zitafanyika kama vile,kupanda miti,
kuhamasisha wananchi kwa njia ya maonyesho ya sinema,kuzindua kitabu cha uenezi kuhusu mazingira.

Matiku alisema kuwa kaulimbiu imekuja wakati muafaka ambapo Taifa letu linatekeleza Programu ya ‘Kilimo Kwanza'ambacho, pamoja na mambo mengine, hufanikishwa na ardhioevu,hususan kilimo cha umwagiliaji.

Alisema kutokana na hali hiyo, Waziri amewahimiza wananchi kutunza vyanzo vya maji na kutofanya
shughuli zozote katika sehemu hizo, kama vile kulima na kuchungia mifugo katika misitu inayohifadhi maji.

Hata hivyo alisema waziri alisisitiza utunzaji wa ardhioevu sharti uambatane na utunzaji wa misitu maana miti na mimea husaidia maji kunywea ardhini na baadaye kutokeza juu ya ardhi kama vyanzo vya maji na huingia kwenye ardhi na kuwepo kwa visima, mito na mabwawa.

No comments:

Post a Comment