01 February 2013

Hoja ya Mbatia imeona mbali



JANA Mbunge wa kuteuliwa kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia, aliwasilisha hoja binafsi bungeni
mjini Dodoma iliyoainisha suala zima la udhaifu uliopo katika
sekta ya elimu nchini.


Katika hoja hiyo, Bw. Mbatia alisema kukosekana kwa mitaala katika shule za msingi na sekondari, kunachangia wanafunzi
kufanya vibaya.

Alisema hali hiyo inachangiwa na utendaji mbovu wa kitengo cha kuandaa mitaala hiyo ambacho kimeshindwa kufanya kazi zake ipasavyo na kusababisha usambazaji vitabu kunuka rushwa.

Hoja hiyo iliibua mvutano mkali kwa wabunge ambao baadhi yao walishauri iundwe Kamati Teule ya Bunge kuchukuza udhaifu huo na wengine wakitaka hoja hiyo ifanyiwe kazi na Serikali.

Ulimwengu mzima unatambua kuwa, hakuna nchi iliyowahi kuendelea bila wananchi wake kuwa na elimu bora. Kwa maana
hiyo, maendeleo yote yametokana na elimu sahihi iliyojaa maarifa, ubunifu, uwezo mkubwa wa kufikiri na kuvumbua dhana mpya.

Elimu inayojenga ujuzi na ufundi wa aina mbalimbali, kudadisi, kujiamini na kutumia fursa zilizopo kutafuta masuluhisho ya matatizo ndiyo inayoleta maendeleo kwenye jamii.

Ni ukweli usiopingika kuwa, wafadhili wametoa pesa nyingi kusaidia nchi masikini ikiwemo Tanzania lakini umaskini
bado unaendelea kuitafuna nchi yetu. Suala la kuwekeza katika
elimu sahihi kwa kuwa na mitaala bora haliepukiki.

Hivi sasa, nchi mbalimbali zilizoendelea zinatafuta maarifa mapya ya kuibadili dunia wapendavyo kwa kurahisisha kila kitu wakitumia teknolojia na uvumbuzi mpya. Hii ndio nguvu ya elimu!


Na hii inazaa changamoto nyingi katika sekta ya elimu, kama vile-

Sisi tunasema kwamba, mitaala tunayoitumia katika shule zetu haiwezi kumjenga mwanafunzi kupata maarifa, ujuzi na stadi
za aina mbalimabali zitakazowasaidia wanafunzi kuishi pindi wamalizapo shule.

Mitaala tuliyonayo haiwafundishi wanafunzi wetu na kuwapa uwezo wa kutatua matatizo yao au kupambana na changamoto zinazoikabili kwenye jamii. Mitaala yetu imetungwa na wataalamu wachache bila kuzingatia mahitaji wa jamii.

Hali hiyo inachangia wanafunzi wetu kukata tamaa na kuwa tegemezi wamalizapo shule na kibaya zaidi, ziara za mafunzo
na kazi za nje zinazokazia maarifa hazifuatiliwi kabisa.

Mbinu za ufundishaji, haziwaelekezi wanafunzi kuwa na ari ya kujifunza, bali zinakaririsha tu. Walimu wengi wanatumia mfumo wa kuandika ubaoni na wanafunzi wananakili maelezo.

Mfumo huu unajulikana kama “ubao-chaki” ambao unawafanya wanafunzi kuwa vikapu vya kupokea maelezo ya mwalimu.

Katika karne hii ya maarifa na changamoto nyingi, mfumo huu haufai. Mbinu shirikishi zinazowapa muda na fursa wanafunzi kujadili wenyewe na kutoa mawazo yao kwa uwazi ndio sahihi.

Mbinu hizo zinaamsha ari ya wanafunzi kujifunza, kudadisi, ubunifu na fikra yakinifu za kukuza uhodari wa kutafuta maarifa hata kama hawapo shule.

Umefika wakti wa Serikali kuweka mikakati ya kifikra ya kuzifanya shule kuwa mahali salama pa kujifunza na kuibua vipaji vya watoto ambapo pengo hili bado halijafanyiwa juhudi za dhati ili kuzibwa.

Hivi sasa mtoto wa masikini anayelilia elimu imkomboe, anahitaji mfumo mzuri ambao utampa dira na dhamira ya kweli ili kuifanya elimu kuwa ni haki ya msingi kwa kila mtoto badala ya watoto wa viongozi pekee.

1 comment:

  1. SI KWAMBA MITAALA HAIPO IPO LAKINI HAITEKELEZEKI TULIKUWA NA AZIMIO LA ARUSHA LILILOZAA ELIMU YA UJAMAA NA KUJITEGEMEA SASA AZIMIO LA ZANZIBAR LINALOHUBIRI ELIMU YA SOKO HURIA KILA KITU NI BIDHAA YA KUUZWA KUJITOLEA NI DHAMBI KUBWA

    ReplyDelete