18 February 2013
Dowans yaibana TANESCO mahakamani
Na Rehema Mohamed
KAMPUNI ya Kufua Umeme ya Dowans, jana iliwasilisha pingamizi la awali katika Mahakama ya Rufaa Kanda ya Dar es Salaam, kupinga ombi la Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kuomba kuzio la utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu.
Mahakama hiyo ilitoa amri kwa TANESCO kuilipa kampuni
hiyo zaidi ya dola za Marekani milioni 65.
Pingamizi hilo liliwasilishwa mahakamani hapo jana na wakili anayeiwakilisha Dowans, Bw. Kenedy Fungamtama, mbele ya Majaji watatu wanaosikiliza shauri hilo wakati lilipoletwa kwa
ajili ya kusikilizwa ombi la zuio.
Majaji hao ni Steven Bwana, Benard Luanda na Edward Rutakangwa, ambaye ni Mwenyekiti wa jopo hilo.
Akitoa sababu za pingamizi hilo, Bw. Fungamtama alidai maombi ya TANESCO kuomba zuio hilo yaliwasilishwa mahakamani hapo nje ya muda ambapo kanuni za Mahakama ya Rufaa zinaelekeza maombi hayo kuwasilishwa ndani ya siku 60 tangu kutolewa
taarifa za kusudio la kukata rufaa.
Alidai shirika hilo liliwasilisha maombi hayo baada ya siku 351 tangu wawasilishe kusudio la kukata rufaa mahakamani hapo
hivyo aliomba maombi hayo yatupwe kwa gharama.
Akijibu hoja hizo, mmoja kati ya mawakili wanaoiwakilisha TANESCO, Bw. Richard Rweyongeza, alidai kanuni aliyoitumia
Bw. Fungamtama, tafrisi yake inaipa mamlaka Mahakama Kuu kusimamisha utekelezwaji wa amri hiyo.
Aliongeza kuwa, tayari walipeleka maombi ya kusimamisha kuilipa Dowans zaidi ya dola za Marekani milioni 65 katika Mahakama Kuu lakini maombi yao yalitupwa na kuamua kuyapeleka Mahakama ya Rufaa siku 13 tangu yalipotupwa.
Baada ya kuwasilishwa hoja hizo, jopo la Majaji liliahirisha shauri hilo hadi watakapopanga tarehe ya kutoa uamuzi wa hoja hizo.
Wakati huo huo, Bw. Fungamtama aliiomba mahakama hiyo itupilie mbali kusudio la kukata rufaa liliwasilishwa mahakamani hapo na TANESCO kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC).
Mahakama hiyo iliitaka TANESCO kuilipa Dowans zaidi ya dola
za milioni 65 ambapo Bw. Fungamtama alidai kuwa, kusudi hilo la kukata rufaa limewasilishwa mahakamani hapo nje ya muda ambapo tayari siku 60 zinazotambulika kisheria zimeshapita.
Akijibu hoja hizo, wakili wa TANESCO Bw. Rweyongeza, alidai walichelewa kukata rufaa kwa sababu Mahakama Kuu ilichelewa kuwapa nyaraka muhimu zinazohitajika kuambatanishwa katika rufaa yao.
Miongoni mwa nyaraka hizo ni pamoja na nakala ya hukumu, mwenendo wa kesi na waliandika barua kwa msajiri wa mahakama hiyo kuomba nyaraka hizo lakini hajawapa majibu hadi sasa.
Novemba 15,2011, ICC chini ya Mwenyekiti wake, Bw. Gerald Aksen na wasuluhishi Bw. Swithin Munyantwali na Bw. Jonathan Parker, iliiamuru TANESCO iilipe Dowans fidia ya kiasi hicho
cha fedha kwa kuvunja mkataba kinyume cha sheria.
Dowans ilisajiri tuzo waliyopewa na ICC ya kulipwa fedha hizo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaa ambayo iliiamuru TANESCO itekeleze amri iliyotolewa na ICC.
Hata hivyo, TANESCO waliwasilisha tena mahakamani hapo ombi la kuomba zuio la utekelezaji wa amri hiyo lakini mahakama hiyo ilidai haina uwezo wa kusikiliza ombi hilo hivyo waliamua kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment