05 February 2013

DC Temeke awafunda wanafunzi Mgulani


Na Charles Lucas

MKUU wa Wilaya ya Temeke Bi.Sophia Mjema amewashauri wanafunzi kutojiingiza katika matendo maovu yanayochangia ukosefu wa madili na kupunguza kiwango cha ufaulu.

Akizungumza jana Dar es Salaam wakati wa mahafali ya 19 ya kidato cha Sita katika shule ya Sekondari ya Jitegemee Mgulani, alisema kumekuwapo na vitendo vya ukosefu wa maadili unaosababisha baadhi ya wahitimu kukosa sifa za uongozi na kushindwa kufanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho.

"Mnatakiwa kujituma katika kwa kusoma zaidi na kuwa na taaluma nzuri badala ya kujiingiza katika vitendo visivyo na manufaa vinavyochangia kushindwa kufanya vizuri katika mitihani ya mwisho, " alisema.

Bi.Mjema aliwataka wahitimu kuwa wawakilishi wazuri wa shule huko wanakokwenda kwa kuachana na vitendo viovu ikiwamo matumizi ya bangi, dawa za kulevya na ngono ili kuwa raia wema na watakaokuwa na tabia njema ndio watakaopewa kipaumbele cha kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Akijibu risala ya shule hiyo kuhusu matatizo mbalimbali yakiwamo ya kukatika mara kwa mara kwa umeme alisema kero hiyo ipo katika nafasi yake na kuahidi kuifanyiakazi .

"Kero nyingine nitazitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na uongozi wa shule hiyo ikiwa ni pamoja na kutafuta wafadhili mbalimbali, " alisema.

Awali akitoa taarifa ya shule hiyo,Mkuu wa shule  Luteni Kanali Martin Mkisi,alisema jumla ya wahitimu 386 wamehitimu wasichana wakiwa 127 na wavulana 259 na kuongeza kuwa kiwango cha taaluma kimepanda.

Mkuu huyo aliwaasa wahitimu hao kuwa safari ya kutafuta elimu ni ndefu hivyo wawe tayari kupambana katika mazingira yoyote lengo likiwa ni kufaulu vema katika mitihani itayofanyika hivi karibuni pia aliwashukuru wazazi kwa ushirikiano waliowapatia mpaka kufikia hatua ya kuhitimu.

No comments:

Post a Comment