18 February 2013

CCM Dar kuwajibu upinzani



Na Rehema Maigala

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeandaa mikutano miwili ya hadhara itakayofanyika jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Temeke Mwisho na Kata ya Goba, wilayani Kinondoni.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Siasa na Uenezi jijini humo, Bw. Juma Simba Gadafi, alisema lengo la mikutano hiyo ni kuzungumzia utekelezaji ilani ya CCM.

Alisema mikutano hiyo itahudhuriwa na viongozi wa CCM Mkoa
na Taifa, Mawaziri, Wabunge, Mameya, Madiwani, makada wa chamaa hicho na wananchi mbalimbali.

“Katika mikutano hii, kutakuwa na upokeaji wanachama wapya ambao wanajiunga na chama chetu kutoka upinzani, mkutano wa kwanza utafanyika Viwanja vya Temeke Mwisho.

“CCM ndio chama pekee kinachozingatia misingi ya amani na utulivu hivyo ni wazi kuwa wanachama wengi kutoka upinzani watajiunga na chama chetu,” alisema Bw. Gadafi.

Aliongeza kuwa, mkutano wa kesho utafanyika Goba, katika Jimbo la Ubungo ambapo chama hicho kitazungumza na wananchi kuhusu mambo mbalimbali maendeleo hasa tatizo la maji.

Alisema kata hiyo inakabiliwa na tatizo kubwa la maji hivyo mkutano huo utatoa majibu ya tatizo hilo kwani hakuna kiongozi yeyote kutoka upinzani anayeweza kulimaliza.

“Kabla mikutano hii haijaanza, viongozi wa chama watafungua matawi mapya ya CCM katika Wilaya za Temeke na Kinondoni,
wanaomba wananchi wapenda amani, wajitokeze kwa wingi
kusikiliza sera za chama na kupatiwa majibu ya matatizo yao,”
alisema.

No comments:

Post a Comment