18 February 2013

Askofu Mokiwa aishukia serikali



Na Yusuph Mussa, Handeni

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dkt. Valentino Mokiwa, ameitaka Serikali kurejesha mali zote za kanisa hilo
ambazo zilitaifishwa wakati wa Azimio la Arusha.


Alisema inasikitisha wanapoziona mali hizo zikiwa katika hali
mbaya kiasi cha kushindwa kufikia lengo lililokusudiwa.

Askofu Mokiwa aliyasema hayo mjini Handeni, mkoani Tanga, mwishoni mwa wiki katika hafla ya kukabidhi chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Mtakatifu Francis iliyopo Kijiji cha Kwamkono, Tarafa ya Sindeni, inayomilikiwa na kanisa hilo.

“Serikali irudishe mali za kanisa...tunaumia tunapoona nyingine
zina hali mbaya...kwa hili hatutaacha kusema,” alisema Askofu Mokiwa na kutaja baadhi ya mali zilizotaifishwa kuwa ni shule,
hospitali na vyuo kikiwemo Chuo cha Ualimu Korogwe.

Alisema Taifa lenye nguvu ni lile lenye watu wenye afya njema  lakini inasikitika kuona baada ya miaka 50 ya Uhuru nchini, bado kuna wanawake wajawazito ambao wanafariki dunia wakati wa kujifungua akiifananidha hali hiyo na dhambi kubwa.


Aliongeza kuwa, kanisa hilo limehangaika sana na wananchi wa Handeni na kuipongeza Serikali kwa ushirikiano ambao imekuwa ikiuonesha kwa taasisi za dini.

“Sisi tunathamini watu wote bila kujali dini zao,” alisema Dkt. Mokiwa na kuishauri Serikali, inapoona kuna matatizo sehemu,  ishirikiane na taasisi za dini kuyapatia ufumbuzi.

Askofu huyo alisema hakuna sababu kwa Serikali kuwa na mashindano na taasisi za dini, kwani ushirikiano ndiyo kitu cha msingi katika  kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya pamoja na elimu," alisema

Aliongeza kuwa wao wapo tayari kupata wataalam kutoka nje kuja kufanyakazi nchini kwa kujitolea, hivyo wakija Serikali isikimbilie kuwatoza kodi.

"Kuna maeneo ambayo Serikali inakosea, unakuta mtu anajitoa kafara anatoka kwao kwenye baridi kuja kusaidia Mzigua, lakini Serikali inamtoza kodi, hili nalo si sawa sawa," alisema Mokiwa ambaye pia ni mwenyeji wa wilaya hiyo.

Aliishauri Serikali iruhusu taasisi za dini zifanyekazi ambazo yenyewe haiziwe ikiwemo kuendelea kutoa huduma za elimu afya na maji.

1 comment:

  1. hii siyo nchi ya dini.hayo unayosema si lazima ushirikishe serikali kama ni kwa nia njema ya kusaidia wananchi.

    ReplyDelete