29 January 2013

Mpina alipuka utoroshaji tril. 11.6/- *Aitupia lawama serikali, apeleka hoja bungeni


Na Benedict Kaguo

MBUNGE wa Kisesa, mkoani Simiyu, Bw. Luhaga Mpina (CCM), amefichua mpango wa Serikali kuwalinda viongozi walioficha fedha katika benki zilizopo nje na kusababisha umaskini kwa Watanzania.

Alisema kitendo cha kuondolewa kipengele kinachozungumzia  utoroshaji fedha zaidi ya sh. trilioni 11.6, kwenye mpango wa maendeleo wa miaka mitano uliopitishwa na Bunge, inaonesha Serikali haina nia ya kurejesha fedha zilizofichwa na wajanja.

Bw. Mpina aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, kutokana na hali hiyo amedhamiria kuwasilisha hoja binafsi katika Mkutano wa Bunge unaoanza leo mjini Dodoma ili Serikali iwaeleza Watanzania kwanini kipengele hicho kimeondolewa.

“Kwa kutumia kifungu cha 55 cha kanuni za Bunge toleo la 2007, tayari nimepeleka barua kwa Spika kumweleza kuwa, kipengele kilichokuwa kwenye mpango huo hakijawahi kuondolewa na
Bunge... lakini Serikali imekifuta wakati Watanzania wanataka
mjadala huo uendelee ili fedha hizo zirejeshwe,” alisema.

Aliongeza kuwa, kwa kutambua unyeti wa suala hilo barua yake ameipeleka kwa Spika Januari 23 mwaka huu, kutaka hoja hiyo ijadiliwe bungeni ili kujua sababu ya kufutwa kipengele hicho.

Alisema Bunge la Aprili 2011, lilipitisha mpango wa maendeleo wa miaka mitano na kipengele hicho kilikuwepo kikizungumzia suala la utoroshaji fedha nje hivyo ni jambo la kushangaza kuona mwaka 2012, wakati akisoma mpango huo bungeni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Bw. Stephen Wassira, kipengele hicho kilikuwa kimeondolewa.

Bw. Mpina alisema tatizo la ufisadi haliwezi kumalizika kama Serikali haioneshi nia ya dhati ya kupambana na vitendo hivyo ambavyo vinawaumiza wananchi masikini nchini.

“Bunge litahoji kwa nini kipengele cha utoroshaji fedha nje ya nchi kiliondolewa wakati Serikali inasema ina dhamira ya kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa nchini,” alisema Bw. Mpina

Hata hivyo, katika Bunge la Bajeti 2012/2013, Bw. Mpina aliikataa bajeti ya Serikali kwa sababu ya kutoweka fedha za kutosha katika shughuli za maendeleo huku akifichua utoroshaji wa sh. trilioni 11.6 uliofanywa kuanzia mwaka 1979 hadi 2008.


1 comment:

  1. MPINA UNAPOTEZA MUDA WAKO TANGU LINI SIMBA AKAMLA SIMBA MWENZIE WEWE NI MWANACHAMA MTIIFU WA CHAMA CHA MAGAMBA MAGAMBA HAYOHAYO NDIYO YANATOLOSHA MABILIONI HAYO UNAYOYASEMA NA WANYAMA PORI,MADINI NK SASA WEWE HUONI UNAFANYA USALITI KWA MAGAMBA WENZIO ACHA UNAFIKI KAMA KWELI UNAHURUMA NA SISI WANYONGE JITENGE NAO TUTAKUELEWA KELELE ZAKO HIZO ZITAKUGHARIMU 2015 MULIZE MWENZIO KIMARIO ALIYEKUWA MBUNGE WA VUNJO NINI KILIMPATA.

    ReplyDelete