29 January 2013

DC Korogwe ategwa kwa magogo


Na Yusuph Mussa, Korogwe

MSAFARA wa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, Bw. Mrisho Gambo, juzi uliwekeza magogo barabarani na kusababisha taharuki kubwa kwa watu waliokuwa katika msarafa huo.


Magogo hayo yaliwekwa kwenye Kitongoji cha Kwemshai- Miembeni, wakati Bw. Gambo na msafara wake wakitoka Kijiji
cha Kizara, Kata ya Kizara, Tarafa ya Magoma, kukagua
maendeleo ya zahanati ya kata hiyo.

Msafara huo ulikuwa ukienda Kijiji cha Bombo-Majimoto, kuzungumza na Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Kizara
ukiwa na magari manne.

Katika msafara huo, alikuwepo Mbunge wa Korogwe Vijijini,
Bw. Stephen Ngonyani, Kamati ya Ulinzi na Usalama ambao
wote walihofia kutekwa na majambazi.

Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama walishuka na kwenda kutoa magogo hayo ambapo baadaye ilibainika kuwa, vijana walioweka magogo hayo walikuwa wanataka kupewa fedha
na viongozi waliokuwa katika msafara huo.

Pamoja na vijana hao kudai wao hawakuhusika kuweka magogo hayo, tisa walikamatwa wakiwemo waliokuwa wakinywa pombe
ya kienyeji 'boha',  chini ya Mwembe na kupakiwa katika gari la
Bw. Gambo, lenye namba STK 3837, gari la Ofisa Usalama wa
Taifa, wilayani humo T 775 BFP na gari la Halmashauri ya
Wilaya SM 3842.

Baadhi ya vijana hao walimtaja mwenzao Bw. Juma Mgosi ambaye alifanikiwa kukimbia na kudai ndiye aliyeweka magogo hayo.

Hata hivyo, vijana hao waliongozana na msafara huo hadi Kijiji cha Bombo-Majimoto ambapo kulikuwa na mkutano wa hadhara na kuachiwa saa moja usiku wakati msafara ukiondoka kurudi mjini Korogwe baada ya Bw. Nyonyani kumuomba Bw. Gambo awaachie.

Baadhi ya vijana hao walijikojolea katika magari waliyopatika ambapo Bw. Ngonyani alidai kuwa, vijana hao aliwazoesha
vibaya kwani kila anakopita barabara hiyo huwapa fedha
lakini njia waliyotumia siku hiyo kuweka magogo si sahihi.

“Nimeambiwa wale vijana walikuwa wanataka pesa ndio maana waliweka magogo wakati msafara ukipita lakini njia waliyotumia
haikuwa sahihi walifanya makosa,” alisema Bw. Ngonyani.

2 comments:

  1. HIYO NI RUSHWA BWANA NGONYANI IWAPO VIJANA MUNASHINDWA KUWAHAMASISHA WAFANYE KAZI KULIKO KUTEGEMEA HELA ZA BURE IKUMBUKWE WANAOZALISHA MAZAO NI AJUZA NA SHAHIBU AMBAO NI CHOKA MBAYA WAELEZE SHAROBARO WAKO HAYO SI MAISHA

    ReplyDelete
  2. Kazi ya kuwapa pesa hao vijana alipewa na nani? na je bajeti yake ilipitishwa na nani? je ni za kwake au za serikali? vijana kweli walikosea LAKINI CHANZO CHA MAKOSA ni nani? ni huyo huyo Mkuu wa wilaya. Kama akifuata uongozi bora hakuwa na haja ya kuwapa fedha, AWAELEZE NAMNA YA KUPATA FEDHA

    ReplyDelete