29 January 2013

CCM yajitosa sakata la gesi *Kinana adai wananchi Mtwara wana hoja *Nape asisitiza rasilimali kunufaisha wote *53 wafikishwa kortini, Nchimbi atoa agizo


Na Waandishi Wetu, Mtwara na Dar

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Abdulrahman Kinana, amesema wananchi mkoani Mtwara wana hoja ya msingi kupinga ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam, hivyo wanahitaji majibu sahihi ya kuwaridhisha.

Bw. Kinana aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye  kipindi cha 'Power Breakfast', kinachorushwa na Redio Clouds akiwa mkoani Kigoma alikwenda kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM.

Alisema wananchi hao wana hoja ambayo hivi sasa imerukiwa na wanasiasa wakidhani wanaikomoa CCM wakati wanaoumia ni wananchi.

“Hoja ya wananchi ya Mtwara ni ya msingi japo imerukiwa na wahuni na kuanza kuchoma magari ya watu, wana Mtwara
wanahitaji majibu ya kile wanachokihoji,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, alisema msimamo wa chama hicho ni rasilimali zote za nchi kunufaisha Watanzania wote.

“Mimi ni mtu wa Kusini, kama ningezuiwa nisitoke ndani ya Mkoa wangu hata shule nisingesoma...naiomba Serikali iwachukulia hatua bila huruma watu wote waliohusika na uchomaji moto magari na kuharibi mali,” alisema Bw. Nnauye.

Wakati huo huo, miili ya watu wanne waliouawa na polisi kwa kupigwa risasi wilayani Masasi, imezikwa juzi katika makaburi
ya Masasi Mbovu, Nyasa na Upanga kati ya saa nne asubuhi
na 10 alasiri.

Maiti mbili kati ya hizo, moja imetambuliwa kwa jina la Jofrey Banabas na nyingine imefahamika kwa jina la Imrani.

Wakizungumza na waandishi wa habari, ndugu wa marehemu Simonje, walilaani kitendo cha polisi kutumia risasi za moto
kutuliza ghasia na kusababisha mauaji.

“Inakuwaje askari aliyepata mafunzo wanapambana na raia wasio
na silaha kwa kutumia risasi za moto, wao walipaswa kutumia
mbinu za kukabiliana nao si vinginevyo,” walisema.

Miili ya marehemu hao imekutwa na matundu ya risasi  tumboni, kifuani, kitovuni, mgongoni na maeneo mengine ya mwili.

Katika vurugu hizo, watu 13 akiwemo polisi mmoja aitwaye Hosea Kibona, wameumizwa vibaya sehemu mbalimbali ya miili yao na kulazwa Hospitali ya Mission ya Ndanda.

Kati ya majeruhi hao, 12 bado wamelazwa hospitalini hapo wakiendelea na matibabu wanne kati yao wapo mahututi na
mmoja aliyeumia bega la kushoto alitibiwa na kuruhusiwa.

Waziri Pinda

Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, jana aliwasili mkoani humo kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali pamoja na wawakilishi wa wananchi ili kutafuta suluhu ya mgogoro
huo akiwa katika ziara ya siku mbili kuanzia jana.

Katika ziara hiyo, Bw. Pinda alichukua maoni ya viongozi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wafanyabiashara ambao wengi wao walitaka Serikali isitishe uamuzi wa kusafirisha gesi kutoka mkoani humo kwenda jijini Dar es Salaam.

Wawakilishi wa wananchi walidai kuwa, hawaoni umuhimu wa Serikali kusafirisha gesi hiyo kwenda Dar es Salaam hivyo ni
bora itafute uratatibu mwingine.

Baadhi yao waliiomba Serikali kumwondoa Mkuu wa Mkoa huo kwa madai ya kushindwa kusimamia suala hilo kikamilifu na
kutetea gesi hiyo isisafirishwe.

Taarifa iliyotufikia wakati tukienda mtamboni, inadai kuna tetesi kuwa Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli wanatarajia kuwasili mkoani humo leo ili kuongeza nguvu ya kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

Watumishi Mtwara

Watumishi wa idara mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, jana walijikuta wakisota nje baada ya ofisi zao kuteketezwa kwa moto kutokana na vurugu zilizotokea hivi karibuni.

Baadhi ya watumishi hao walionekana wakichambua mabaki ya nyaraka ambazo ziliungua moto.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wenzake, Ofisa Elimu Taaluma wa Shule za Msingi, wilayani humo, Garama Kinderu alisema wamelazimika kukaa nje baada ya ofisi yao kuchomwa
moto na vijana waliokuwa wakiandama kupinga mwendesha
pikipiki 'bodaboda, kukamatwa na polisi.

Alisema idara ya elimu imeathirika kwa kupoteza kumbukumbu
za walimu, wanafunzi na taarifa za maendeleo ya elimu baada
ya kuungua kwa kompyuta zilizokuwa zikitunza kumbukumbu.

Watuhumiwa 53

Katika hatua nyingine, watuhumiwa 53 wanaodaiwa kuhusika na vurugu zilizotokea wilayani humo, jana wamefikishwa kwenye mahakama ya Wilaya na kusomewa mashitaka yao likiwemo
la kula njama, kutenda kosa la kuchoma moto majengo ya halmashauri ya wilaya na uharibifu wa mali.

Wakisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Elizabert Nyembele, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Bw. Daniel Samuel, alidai kwa nyakati tofauti watuhumiwa walitenda kosa la kuchoma moto majengo na uharibu mali.

Alidai washtakiwa waliichoma moto Ofisi ya CCM Wilaya, Mahakama ya Mwanzo Lisekese, Ofisi ya Idara ya Elimu, Msingi
na Sekondari, Maliasili na Wanyama pori, magari ya halmashauri,
nyumba za raia na viongozi ikiwemo ya mbunge wa Masasi,  Mariamu Kasembe na Anna Abdallah.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 11 mwaka huu na watuhumiwa wamerudishwa rumande baada ya upande wa Serikali kupeleka pingamizi la washtakiwa kupewa dhamana.

Ziara ya Dkt. Nchimbi

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, jana alifanya ziara ya kukagua majengo ambayo yameteketea kwa moto kutokana na vurugu hizo.

Katika ziara hiyo, Dkt. Nchimbi aliongozana na Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Bw. Paul Chagonja pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mngulu.

Dkt. Nchimbi aliliagiza jeshi hilo wilayani humo kuhakikisha kuwa, wote waliohusika katika uharibifu huo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Tukio hili limenisikitisha sana kwani ni la aina yake kutokea hapa nchini, uharibifu wa mali umekuwa mkubwa pamoja na nyaraka za Serikali hivyo kusababisha hasara kwa Taifa,” alisema.

“Hatuwezi kuacha vitendo hivi vinaendelea kuharibu amani, mali za watu na Serikali, naliagiza Jeshi la Polisi wilayani hapa kuusaka mtandao unaofanya vitendo hivi,” alisema Dkt. Nchimbi.

Hasara ya mali

Katika vurugu hizo, magari, majengo ya watu binafsi na taasisi za Serikali, yaliharibiwa vibaya kwa kuchomwa moto ambapo hadi
sasa, hasara iliyotokana na uharibifu huo bado haijafahamika.

Vurugu hizo zinazodaiwa kufanywa na vijana wenye umri chini ya miaka 40 kwa madai ya kuchoshwa na tabia ya baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi kunyanyasa wananchi hasa vijana wakiwemo waendesha pikipiki za abiria wilayani Masasi.

Majengo nane yaliharibiwa katika vurugu hizo na magari 11 zikiwemo nyumba tatu za kuishi zinazomilikiwa na Bi. Mariamu Kasembe, Bi. Anna Abdallah na polisi wa Usalama Barabarani
aliyefahamika kwa jina la Mussa Kero.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Maria Nzuri, ameitaka jamii kutojihusisha na masuala ya vurugu ili kudumisha amani iliyopo nchini na kama wana madai, watumie njia zinazokubalika kudai
haki zao badala ya kufanya vurugu na kuharibu mali.

Upatikanaji mahitaji

Kutokana na vurugu kubwa zilizotokea juzi wilayani humo, baada ya kundi la waendesha pikipiki za kubeba abiria 'bodaboda', kufanya maandamano wakipinga kukamatwa na polisi, kutozwa faini zisizo lingana na makosa halisi, hali hiyo imesababisha upatikanaji wa huduma za msingi kuwa mgumu.

Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema hali ya upatikanaji mahitaji ya msingi ni ngumu kutoikana na maduka pamoja na vipanda vinavyotoa huduma kufungwa siku mbili mfululizo tangu kutokea vurugu hizo.

“Tumekuwa tukihangaika kutafuta bidhaa mbalimbali bila mafanikio hivyo kusababisha ugumu wa maisha,” alisema Bw. Mohamed Rajanu na kuongeza kuwa, bidhaa zisizopatikana kirahisi ni
vocha za simu, mchele, sukari, ngano, mafuta ya kupikia.

Imeandikwa na Reuben Kagaruki, Said Hauni, Cornel Anthony na Hamisi Nassir.

2 comments:

  1. HIVI KAULI YA MBOWE WA CHADEMA KUWA KAMA NOMA NAIWE MOMA IMEMUONDOLEA UTU NA UBINADAMU JE WATU NANE WALIOKUFA KUMI WALIOJERUHIWA HIVI NANI ANAHUDUMIA FAMILIA ZA WAHANGAWAKATI ANASEMA HIZO NI MVUA ZA RASHARASHA BADO VURUGU ZITAKUWA NCHI NZIMA MAENGO MANANE NA MAGARI KUMI NA MOJA YALIYOCHOMWA MOTO NANI ATAYALIPA HIVI KWANINI USISHITAKIWE THE HAGUE AU KWA KUWA WANASHERIA WA KITUO CHA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA A.K.A CHAMA KISICHO NA USAJIRI WANAFANYA KAZI KISIASA

    ReplyDelete
    Replies
    1. YA MTWARA HAYAUSIANI NA MBOWE MSITAFUTE MCHAWI WANALINDI NA MTWARA WAMEAMUKA KUTOKA KTK USINGIZI MZITO WALIOKUWA WAMEFUNIKWA NA BLANKETI ZITO LA KIJANI NA NJANO LENYE NEMBO YA JEMBE NA NYUNDO KUZINDUKA WAKAKUTA WAMEBAKI WENYEWE NYUMA KIMAENDELEO UKILINGANISHA NA WATU WA MIKOA MINGINE TZ WAKATAFUTA ALIYEWAFUNIKA HIYO BLANKETI WAKAGUNDUA KUMBE NI MAGAMBA (ccm) KWAHIYO NDUGU YANGU YANAYOJIRI MTWARA NA LINDI SI KAULI ZA KAMANDA MBOWE BALI ZINATOKANA NA TOFAUTI ZA KIPATO KATI WACHACHE (WATAWALA) NA WENGI WALALAHOI AMBAO NDIO WANADAI HAKI ZAO ZA MSINGI .

      Delete