29 January 2013

Bulembo amshukia Bujugo



Na Gladness Mboma

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Bw. Abdallah Bulembo, amemtaka Diwani wa Kata ya Magomeni Dar es Salaam, anayeendesha Chuo cha Kilimo cha Kaole, kilichopo Bagamoyo, mkoani Pwani, Bw. Julian Bujugo, kukikabidhi chuo hicho kwa jumuiya hiyo kabla hajachukuliwa hatua za kisheria.


Bw. Bulembo alitoa agizo hilo wakati akijibu maswali ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), wilayani humo, Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Jumuiya ya Wanawake (UWT) na Mabaraza ya Wazazi kwenye kikao cha ndani.

Wajumbe hao walitaka kufahamu hatima ya chuo hicho kurudi mikononi mwa jumuiya hiyo ambapo Bw. Bulembo alisema,
uamuzi wa jumuia hiyo kumuondoa Bw. Bujugo katika chuo
hicho uko pale pale kwani hana haki kisheria ya kuendelea
kuwepo eneo hilo na kufanya ujenzi kiholela.

“Bujugo aliingia hapa kijanja, mikataba yake ni feki, haina baraka za Baraza Kuu la Wadhamini la Wazazi, lakini kibaya zaidi anaendelea na ujenzi bila kuwa na kibali kutoka wazazi au halmashauli hili ni kosa lingine.

“Kabla sijachukua hatua nyingine za kisheria, nakuagiza Ofisa
Ardhi uliopo hapa, usimamishe mara moja ujenzi unaoendelea, lazima Kaole iendelee kuwa ya Wazazi kama ilivyokuwa awali maana ina historia kubwa kwa wakazi wa Bagamoyo, chama na Serikali,” alisema Bw. Bulembo.

Bw. Bujugo anadaiwa kukabidhiwa shule ya sekondari na Ufundi Kaole ili kuiendesha kama Meneja wa shule lakini alikiuka makubaliano na kuigeuza shule hiyo kuwa Chuo cha Kilimo.

“Nawahakikishia kipimo changu cha uongozi katika jumuiya
hii, mtakiona katika suala hili ili jumuiya ipate haki yake kwa kurudishiwa shule yake ambayo hivi sasa ni chuo.

“Tukiwa mjini Dodoma wakati Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete akifunga mkutano wetu wa uchaguzi, alidai kukerwa na hali ilivyo sasa katika shule hii yenye historia
kubwa katika nchi yetu.

“Leo hii majengo ya kihistoria yamevunjwa jambo ambalo si kwamba limemkera Rais wetu pekee, hata wananchi ndani na
nje ya Bagamoyo,” alisema Bw. Bulembo.

Kwa upande wake Mjumbe wa NEC, wilayani humo Bw. Ridhiwani Kikwete, alisema hakubaliani na mikataba iliyopo kati ya wazazi na Bw. Bujugo.

“Nakushukuru sana Mwenyekiti kwa kuliona hili, lakini niwaulize ndugu zangu ni kweli tunashindwa kuchukua hatua hadi mgeni aje ndipo tuseme matatizo yetu,” alihoji Bw. Kikwete.

Alisema yeye kitaaluma ni Mwanasheria na haelewi kitu kuhusu mkataba huo ambapo Bw. Bujugo hawezi kuliendeleza eneo hilo
bila kibali hivyo alimuunga mkono Bw. Bulembo na kusisitiza
kuwa, Wilaya hiyo ina maatatizo kwa Maofisa wa Ardhi ambao
wamekuwa wakifanya kazi kinyume na maadili.

Aliongeza kuwa, baadhi ya watendahi wameifanya wilaya hiyo kama 'shamba la bibi', kwa ajili ya kufanikisha mipango yao ya kudhulumu ardhi za wananchi na kuwaacha wakitaabika kutafuta
haki zao na wengine kupelekwa mahakamani kwa kudai haki.

Awali wananchi hao waliulalamikia uongozi wa halmashauri hiyo kutokana na vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watendaji wake hususan Idara ya Ardhi kuuza ardhi ya wananchi bila ridhaa yao.

Kwa upande wake, Bujugo alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, alisema hawezi kuzungumza lolote ila anaamini chuo hicho anakiendesha kisheria na ana mikataba yote inayomruhusu
kuwepo eneo hilo.

No comments:

Post a Comment