07 June 2012

Tanzania yapanda viwango vya FIFA


Na Mwandishi Wetu

TIMU ya Taifa (Kilimanjaro Taifa Stars), imepanda katika viwango vinavyotolewa kila mwezi na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kutoka nafasi ya 145 mpaka 139.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura ilieleza kwamba Tanzania imepanda kwa nafasi sita kwenye orodha hiyo inayoongozwa na Hispania.


Alisema timu hiyo ambayo kwa sasa inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, ilikuwa namba 145 hivi sasa imefika nafasi ya 139 ikiwa na pointi 214.

"Mei 26, mwaka huu Taifa Stars ilicheza mechi ya kirafiki na Malawi na kutoka suluhu. Malawi yenye pointi 324 imeporomoka kwa nafasi tano kutoka ya 102 hadi 107," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Alisema Ivory Coast ambayo katika mechi yake ya mwisho Juni 2, mwaka huu iliifunga Taifa Stars mabao 2-0 imeporomoka kwa nafasi moja kutoka ya 15 hadi 16 ikiwa na pointi 943. Hata hivyo ndiyo inayoongoza kwa upande wa nchi za Afrika katika viwango hivyo.

Wakati huohuo, timu ya Taifa ya Hispania imeendelea kuongoza ikifuatiwa na Uruguay, Ujerumani, Uholanzi, Brazil, England, Argentina, Croatia, Denmark na Ureno.

Zingine ni Chile ambayo ipo nafasi ya 11 ikifuatiwa na Italia, Urusi, Ufaransa, Ugiriki, Ivory Coast, Sweden, Jamhuri ya Ireland, Mexico na Colombia.

No comments:

Post a Comment