23 March 2012

Mila na desturi kikwazo maendeleo ya elimu- Rorya


 Baadhi ya wazazi wakicheza ngoma kabla ya kuwapeleka watoto katika unyago.


Na Raphael Okello.
WILAYA ya Rorya Mkoani Mara ni moja ya wilaya changa nchini iliyotangazwa rasmi kuwa na mamlaka yake ya kiutawala kamili mwaka 2007.

Wakati inatangazwa rasmi na kutengwa kimpaka kutoka katika wilaya ya Tarime na Rais ya awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete ilikuwa duni katika nyanja zote.

Uduni huo ulitokana na huduma mbaya katika nyanja za elimu, maji, afya, miundombinu za barabara, umeme, kilimo, mawasiliano na biashara.

Pamoja na changamoto zingine pia imechangiwa na mwamko mdogo katika masuala ya elimu.

Sehemu kubwa wakazi wa wilaya hiyo walitegemea shughuli za ufugaji, kilimo na uvuvi kama shughuli kuu za uchumi.

Hali yao iliendelea kuwa mbaya kiuchumi  mifugo yao ilipotokana na wimbi la ujambazi huku samaki nao wakipungua katika Ziwa victoria kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Hata hivyo kabla ya hapo shughuli hizo zilifanyika katika kiwango cha chini kutokana na elimu ndogo huku mila na desturi zikichukua sehemu kubwa.

Wakati watoto wa kiume walipokuwa wakiandaliwa kuwa wafugaji na wavuvi kwa upande mwingine watoto wa kike waliandaliwa kuwa mama na walezi wa familia.

Sherehe za jadi na masharti ya kimila zilifanywa kuwa sehemu ya mfumo wa maisha zisizobadilika.

Hali hiyo ilifanya jamii kutoona umuhimu wa kupeleka watoto wao shule ambapo, shule za msingi, sekondari na vyuo hazikupata nafasi ya kujengwa ikilinganishwa na wilaya zingine mkoani Mara.

Kutokana na wilaya hiyo kuwa pembezoni hata mashirika ya dini hayakuvutwa kuwekeza katika elimu kwa wakati huo ikilinganishwa na wilaya za Tarime, Musoma vijijini, Bunda na Serengeti.

Mashirika ya dini yaliweza kuwekeza katika maeneo machache hasa katika huduma za afya ambapo Hospitali ya Ka Bwana ilijengwa Shirati na Hospitali ya Dudu Kowaki zote zikiwa ni za misheni.

Hadi Tanganyika tunapata uhuru mwaka 1961 Rorya ilikuwa na  shule moja ya madhehebu ya dini iliyojulikana kama shule ya kati 'Middle School', iliyojegwa na wakoloni na wamisionari kule Minigo katika mji mdogo wa Shirati.

Lakini hata baada ya uhuru serikali ilipoanza kuboresha elimu kwa kujenga shule chache za misingi na Sekondari Wilaya ya Rorya haikupata shule hata moja ya Sekondari.

Hadi katika miaka ya 1990 ilikuwa na shule mbili binafsi ya sekondari ya Michire katika mji mdogo wa Shirati na Isango kule Kinesi.

Ni hao wachache waliopata nafasi katika shule kutoka wilayani Rorya ndio waliowahi kupata elimu na kupata nafasi za uongozi na utumishi serikalini na nje nchi.

Hata hivyo wasomi hao waliowahi kueliminika bado wanalaumiwa kuwa na mchango mdogo wa elimu katika kukuza ufahamu wa wakazi wa Rorya ikidaiwa kuwa wengi wao wanatawaliwa na wivu na ubinafsi.

Hata hivyo shule za kata pekee ndizo zilizoanza kuongoza idadi ya wanafunzi sekondari na kuleta matumaini kwa wakazi wa Rorya kupata elimu ya sekondari katika miaka ya 2000.

Pamoja na kuwepo kwa shule za kata ambazo zinakabiliwa na changamoto nyingi katika utoaji wa elimu bora ufaulu wa wanafunzi wanaojiunga na shule hizo ni ndogo.

Licha ya changamoto ya kukosekana kwa mabweni, kutembea umbali muda mrefu hadi shuleni, upungufu wa vyumba vya madarasa bado inaelezwa kuwa mila na desturi ni tatizo kubwa.

Kijiografia Rorya inapakana na nchi jirani ya Kenya hivyo kuchangia mila na desturi jirani zao ambao ni makabila ya Waluo na Wakurya wa pande zote.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi za kiraia wilayani Rorya Mhandisi Patrober Alando anasema, changamoto ya elimu ni kubwa wilayani humo kutokana na jamii kuendekeza desturi zilizopitwa na wakati.

Baadhi ya desturi zinazochangia kushuka kwa kiwango cha elimu wilayani humo ni pamoja na sherehe za kimila ambazo wanafunzi pia uhusishwa katika sherehe hizo.

Anakemea tabia ya baadhi ya watu kutumia wanafunzi kama 'wanenguaji' kati sherehe za Disco kuwaburudisha wateja wao na kwamba hali hiyo ni hatari kwa maendeleo ya baadaye ya watoto hao.

Anasema, hali hiyo inaendelea kukithiri wilayani humo hivyo hufanya wanafunzi kutumia muda mwingi katika michezo ya muziki badala ya kujisomea.

Utoro umeendelea kukithiri katika shule za misingi na sekondari huku wanafunzi wa kike wakikatishwa masomo kwa kuozwa na wengine kupata ujauzito lakini hata wale wanaofikia kufanya mitihani ya kuhitimu bado ufaulu unakuwa mdogo.

Anasema, hatua pekee ya kukomesha desturi hizo ni kuwapa elimu wazazi na walezi ili wabadili msimamo wao kwa kuona umuhimu wa kuwasomesha watoto.

Bw. Alando anasema kuwa, taaluma ya walimu wengi pia ni ndogo ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo walimu walikuwa na uwezo mkubwa wa kuwafaulisha wanafunzi.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, hali hiyo imetokana na kushuka kwa maadili ya vijana kutokana na athari za utandawazi pamoja na mitaala ya elimu isiyokidhi hitaji ya walengwa.

"Mazingira pia ya utoaji elimu hairidhishi, walimu wenyewe wengi wao leo hawana ujuzi katika masomo hasa ya Sayansi, kiingereza na Hisabati sasa wanafunzi wao watakuwaje".

"Isitoshe, Mwalimu anashirikiana na wanafunzi kucheza disco utadhani hakuna serikali hapa Rorya wakati serikali inaanzia katika Kitongoji hadi mkoani, hawaoni vitendo hivi" anahoji Bw. Alando.

Anasema, Rorya haina hata chuo kimoja cha elimu na kusisitiza vyuo vya elimu kuanzishwa akipendekeza kubadilishwa kwa shule ya Sekondari Isango kuwa chuo cha elimu kutokana na mazingira yake mazuri.

Anasema, sekondari hiyo ina nyumba za kutosha za watumishi, vyumba vya madarasa na mabweni hivyo serikali ingebadili shule hiyo kuwa chuo cha elimu au chuo cha ufundi VETA.

Bw. Benedict Kitenga ni mkuu wa wilaya ya Rorya ambaye anataja changamoto zinazowakabili wanafunzi ni pamoja na jamii hiyo kuendelea kushikilia mila na desturi bila kujali elimu.

Anasema, waliopata elimu ya juu na nyadhifa mbalimbali serikalini ambao ni wazawa wa wilaya ya Rorya ni wachache lakini wengi wao hutokomea katika miji.

Lakini wakati huo wako tayari kufanya harambee kokote waliko kutekeleza masuala ya kimila na kufanikisha mambo ya misiba kuliko kuendeleza elimu ya watoto wao.

"Kwanza wazazi wengi hawako tayari kupeleka watoto wao shule kwa kutoa mali zao wakati ambapo fedha nyingi wanazitumia katika sherehe na anasa mbalimbali" anasema Bw.Kitenga.

Bw. Kitenga anafafanua kuwa, jamii hiyo inaendekeza sherehe huku wanafunzi nao wakihusishwa katika sherehe hizo jambo ambalo anaeleza kuwa ni hatari kwa mustakabali wa watoto hao.

Anahoji sababu za kuendeleza desturi ya kukaa katika matanga kwa muda wa wiki moja na zaidi huku ukoo, ndugu na marafiki wakichanga fedha nyingi za matumizi.

Bw. Kitenga anasikitishwa na hali hiyo ambayo anasema kwa muda wote huo shughuli za anasa zinafanyika ikiwa ni pamoja na sherehe za muziki, vinywaji na hulaji wa aina mbali huku wakishindwa kuwachangia hata wanafunzi wao ambao hawana uwezo wa gharama za shule.

Anawataka viongozi wa kisiasa, madhehebu ya dini kusaidia serikali katika kuimarisha elimu wilayani Rorya ili kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.

Anasema, watoto wa kike hawaelezwi umuhimu wa kwenda shule badala yake wanatumikishwa na kuozwa na wazazi wao katika umri mdogo.

"utawakuta wanafunzi wa kike na kiume wakicheza muziki bila kujali cha ajabu iwe mchana hata usiku sasa watasoma saa ngapi" anahoji Bw. Kitenga.

Anasema, wilaya ya Rorya bado ni changa na fedha nyingi kutoka serikalini bado zinatumika kuimarisha mfumo wa utawala ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu ili kuwezesha huduma kufanyika kwa haraka.

Anawataka wazazi kuona umuhimu kushirikiana na vyombo vingine, mashirika na wahisani katika kuimarisha elimu.

Hata hivyo anasema kuwa, serikali inajitahidi kuimarisha shule za kata ikiwa ni pamoja na kuwaajiri walimu wapya ili kuleta ufanisi katika shule hizo.

Maendeleo ya elimu Rorya inakuwa kwa kiwango kidogo na kwamba ushirikiano pekee wa jamii katika kuishawishi serikali, mashirika ya dini na asasi mbalimbali ndizo zitakazosaidia kukuza elimu wilayani humo.


No comments:

Post a Comment